Jumanne, 1 Agosti 2017

Kijana na Utandawazi



VIJANA NA UTANDAWAZI
Je utandawazi ni nini?
Utandawazi  (Globalization) kama ilivyoelezwa katika Wikipedia;
  • ni kukifanya kitu kuwa katika kiwango cha kimataifa, na kukihamisha nje ya mipaka na kukifanya kuwa cha wazi na kikafanywa na watu wa aina yote duniani.
  • ni njia ambayo taifa moja hufanya mambo kuwa ya kimataifa, kufanya mambo pamoja duniani.
  • ni mfumo wa uhusiano wa kimataifa katika nyanja mbalimbali kama vile biashara, uchumi au siasa uliowezeshwa na maendeleo ya teknolojia ya habari yanayofanya mataifa kuwasiliana kiurahisi
  • Utandawazi pia unalenga katika kumiliki fikra au tamaduni zilizo dhaifu, kwa ajili ya kusaidiana na kuungana yaani kuwa kitu kimoja, kuondoa mipaka na masafa kati ya nchi na nchi, kukusanyika pamoja na kuleta kitu kinachoitwa "kijiji-ulimwengu" (global village).

Kwahiyo utaona kwamba mambo msingi au rasmi yanayohusika na utandawazi ni uchumi, biashara, teknolojia, siasa, utamaduni n.k

Kijana ni nan?
Umri wa miaka (12-35) inawakilisha umri wa kijana.

Kwanini ni muhimu kwa vijana kujua juu ya Utandawazi?

1. Kwa sababu ndio wana nguvu ya kupigana vita vya kimwili na kiroho

(1Yoh 2:14b)-"Nimewaandikia vijana kwa sababu mna nguvu na neno la Mungu linakaa ndani yenu nanyi mmemshinda yule mwovu, msiipende dunia wala mambo yaliyomo ktk dunia, kwa sababu ukiipenda dunia kumpenda baba hakumo ndani yako" na (1Yoh 2-14-3:13) "msistaajabu ulimwengu ukiwachukia (Kaini na Habili)"

Lakini nguvu za kiroho tunapata wapi? (Soma Waefeso 6:10-18).

2. Kwa sababu ukweli ndio utamweka kijana kuwa huru na kuwa na uamuzi juu ya mustakabali wa maisha yake.

Kwa mfano:

-Akijua faida ataweza kukimbizana nazo ili apate kufaidika nazo na
-Akijua hasara zake pia atajiepusha na kubaki katika hali nzuri aliyoumbwa nayo.

 

Hata hivyo hii itategemea malezi (wazazi, walimu, media, jamii n.k.) ya huyu kijana hasa katika namna anavyoweza kutumia uhuru/utashi wake vizuri au vibaya. Wengine wamekosa malezi bora/upendo, wazazi hawajali, jamii haijali shida zao, walimu wanawabagua, media inawabeza (wasio na uwezo) n.k LAKINI hii isiwe sababu kwa kuwa upendo wa Mungu unatosha (1Yoh 3:1)

(mfano tunaweza kuona tofauti ya kijana anayejiingiza kwenye maovu na upande mwingine kijana anayechagua kupigania kupata mazuri na kufanikiwa). Mwisho wa hawa wawili utakuwa tofauti sana na kinyume lakini wote wanapata maarifa kwa sababu ya utandawazi. 

LAKINI AKIJUA vema neno la Mungu ataweza kusimama vema zaidi kwani "Mwenye kuushinda ulimwengu ni nani isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu" (1Yoh 5:5) ..atataka kuwa kama Yesu, na Yesu ni mpole na mnyenyekevu, ana hekima na tumemjua akiwa kijana kama sisi, (e.g. Kuwa na Hisia kama Yesu-Askofu Josaphat Lebulu).

Tumwombe basi ili atufanye tuwe kama yeye (1Yoh 5: 14-15) i.e tukiomba sawa sawa tutapata
 kuwa na kiasi (Tito 2:6).

Je Utandawazi una faida au hasara?
Utandawazi kwa mtizamo wa jinsi ulivyoanzishwa katika miaka ya 1980, unalenga kuboresha ulimwengu kwa kutumia nyenzo au mali ghafi watu na vitu kote ulimwenguni kwa faida ya watu wote ulimwenguni. Hata hivyo pamoja na malengo mazuri hayo tayari kumetokea changamoto mbali mbali kutokana na utandawazi huu na pengine kupelekea madhara makubwa yasiyorekebika kiurahisi.

Faida za Utandawazi
Ni mfumo unaoweza kuleta maendeleo na faida kwa kufungua milango ya kiuchumi kidunia kuwezesha kukua haraka kwa uchumi kutokana na upatikanaji wa vitendea kazi na hivyo kupunguza umasikini

Mfano:
Biashara
Ushirikiano wa uuzaji bidhaa toka nchi moja hadi nchi nyingine utasaidia kuinua uchumi            na kuleta maendeleo-Soko huria (mf. DITF-maonyesho ya sabasaba), kununua kwa kadi, na kulipia huduma mbali mbali kwa kadi na kupunguza kutembea na pesa mkononi kwa ajili ya usalama wa fedha na binadamu.

Uchumi          
Nchi tajiri na watu wenye uwezo duniani kuwekeza mitaji yao katika nchi maskini na kukuza uchumi wa nchi husika (mf. miradi ya gesi, madini, umeme n.k)

Uhuru wa kusafiri  
Watu kusafiri kutoka nchi moja hadi nchi nyingine kutafuta kazi na maisha bora (SA, Kenya, Uganda n.k.). Hii inatoa fursa nzuri kwa ajira, matibabu, kuhubiri Injili, Utalii na mengineyo.
 
Kuenea kwa maarifa (Teknolojia) 
Kuboresha mawasiliano na upashanaji habari (google, BBC, n.k) -Hii imeleta urahisi wa kutafuta na kutuma maombi ya kazi au shule mahali kokote duniani, kuleta maarifa karibu na kila mtu (anayependa maarifa) kupitia mifumo ya internet. Fursa nyingi zinapatikana nchi mbali mbali kwa watu wote na ni wale tu wanaofuatilia wanaopata fursa hizo na kuendelea. 

Tumeona pia namna nyanja hii ilivyoweza kuboresha usomaji mashuleni kwa wale wenye mitandao mashuleni....kwamba mtu anaweza kupakua (download) video za kitaaluma za masomo mbali mbali au notes za masomo mbali mbali na kujifunza hata akiwa hana kitabu. Katika nyanja za afya, kilimo n.k pia kuna mafanikio makubwa katika kuwafikia wahitaji kwa njia hii.


Hasara za Utandawazi

Biashara         
Uwezekano wa mataifa maskini kuzidi kuwa maskini kwa kupeleka bidhaa hafifu sokoni na hivyo kudoda (mf. watu kupenda bidhaa za kigeni na kuona za ndani hafifu hivyo kuzidi kuwadidimiza wananchi/wazawa) wa nchi maskini. Urahisi wa kufanya biashara chafu kama wizi wa kimtandao na biashara hewa zinazoishia kuwaumiza wachache wasioelewa kwa kuahidiwa utajiri ktika mtandao.

Uchumi          
Ukosefu wa sera mathubuti, uzalendo na vitendo vya rushwa vilivyokithiri vimepelekea nchi changa kuzidi kuwa maskini zaidi kwa kuwa mapato stahiki hayafikii nchi husika na huishia kwa watu binafsi. Kwahiyo badala ya kukuza uchumi wa nchi husika inakuza uchumi wa nchi tajiri na watu mmoja mmoja wenye tamaa ya fedha na kukosa maadili. (mf. richmond, escrow n.k)

Uhuru wa kusafiri
Hii pia imepelekea ongezeko la uhalifu wa kimataifa kwa sababu ya uhuru wa namna hiyo. Hata hivyo katika baadhi ya nchi wameendelea kupinga kuingiza wageni na kupata kazi katika nchi zao. Hii inatokana na hofu ya kushindwa kushindana katika soko la ajira. Na hii ni wazi kwa kuwa kama nchi haijaelimisha watu wake halafu ikahitaji watu wenye ujuzi na elimu zaidi katika kazi hapa utakuta wazawa wa nchi husika watabaki mitaani na wageni kupata kazi. (mf. Africa Kusini, Kenya, Uganda n.k.).
Pia kwa uhuru huu vijana wengi wametoroka nchi zao kwa kutafuta urahisi wa maisha nchi za nje na wengi kwa kuwa hawakufuata utaratibu na hawana ujuzi wowote, huangukia kufanya biashara chafu za ngono, madawa ya kulevya na uhalifu mitaani.

Kuenea kwa maarifa - (Teknolojia)
Katika eneo hili vijana wamejikuta katika mkumbo wa kupoteza muda mwingi katika mawasiliano yasiyo na tija na kusababisha kudumaa kwa akili hasa kwa vijana na hivyo kushindwa kumudu changamoto za maisha. Kwa mfano kupitia simu za mkononi, video za mitaani, programu za televisioni zisizo na maadili au zilizokosa mafundisho ya maana na hivyo kuchangia sana kudumaza akili ya vijana na kupelekea kuwa na kizazi kisichofundishika na kuporomoka kwa maadili kusiko kwa kawaida.

Mfano:

-kuangalia picha za ngono, vita na tabia zingine mbaya kama ushoga na kuwafanya vijana waone ni sehemu ya maisha yao.
-Vijana kuhadaika na mitindo ya kimataifa kila kukicha (DRC youth)
-Vijana kuiga utamaduni wa kigeni na kudharau wa kwao

Mwisho wa yote ni kwamba katika kuiga yasiyofaa vijana ambao ndio uti wa mgongo wa taifa hawashiriki tena kazi za maendeleo, uwezo wa kufikiri umeshuka, wanataka vitu rahisi rahisi kama kubofya/kuslide/kutouch n.k, na katika elimu, viwango vinashuka kwa kasi siku hadi siku na hatima yake ni kukosa sifa za kushiriki katika global village..vicious cycle -the digital divide
ukiangalia sana uhalifu nawe huchelewi kuwa mhalifu-au ukiwa shabiki wa jambo fulani hata kwa kulibeza utajikuta siku moja unatenda vivyo hivyo. Angalia mfano wa mafundi ujenzi na lugha wanazotumia, mgeni katika kundi huanza kwa kushangaa hizo lugha na mwisho naye anaona mazoea na kuanza kuzitumia.

Matokeo Mabaya ya Utandawazi kwa vijana
-kutojali kitu chochote (globalisation of indefference - Lack of interest, concern, or sympathy)
-Ulevi na Uasherati uliopindukia kuonekana ni fasheni
-Kujibadilisha Jinsia
-Kusahaulika kwa maadili mema ya Kiafrika katika jamii
-kuathirika kimwili, kiakili na kiroho
-Familia kusambaratika---kanisa je limepona?
-Uhuru uliokithiri kwa watoto/vijana
-Kufifia kwa ubinadamu/utu katika jamii (mfano: kuona mtu akiuawa bila shida na kupiga picha kwa ajili ya kusambaza badala ya kusaidia
-unafiki umeongezek

Mazoea mazuri ndani ya utandawazi
-Wazazi wawe mfano mzuri kwa watoto wote na kukemea watoto ili waache yasiyofaa (simu, mavazi, lugha,ulevi n.k)
-Mtoto wa mwenzio ni wako 
mf. Mama Salma Kikwete alitukumbusha kusaidiana malezi

-Tutumie utandawazi kujipatia elimu bora na huduma mbali mbali kama mpesa, e-learning, kupatana n.k
-Tumpende Mungu kwa moyo wote, akili yote
-Tuepuke kutawaliwa na mawasiliano bali sisi tuyatawale mawasiliano-tusiabudu miungu mingine
-Tutumie mitandao kueneza Injili ya Kristo kwa njia ya blogs, facebook, whatsapp n.k


JE VIJANA WA MUNGU TUFANYEJE?
Fil 4:8-10
Hatimaye ndugu zangu, mambo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo na sifa, yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote ya kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo uzuri wo wote, pakiwepo na cho chote kinachostahili kusifiwa, tafakarini mambo hayo. Mambo yote mliyojifunza au kupokea au kusikia kutoka kwangu, au kuyaona kwangu, yatekelezeni. Na Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi. Tunaona hapa kwamba pamoja na maovu kukithiri  ndani ya utandawazi bado tunalazimika kuchagua yale yanayompendeza Mungu kama yalivyoainishwa na Mtume Paulo.

SWALI? JE MAMBO HAYO YA KWELI NA YENYE SIFA KATIKA ULIMWENGU WETU VIJANA NI YAPI? JADILI


Mathayo 11:28-30
“Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jifungeni nira yangu; jifunzeni kutoka kwangu; kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha nafsini mwenu. Kwa maana nira yangu ni rahisi, na mzigo wangu ni mwepesi.”

Je kijana Mkristo, Utandawazi umekulemea? Umekuwa mzigo kwako? Umekuachia majeraha? Umekuachia mazoea mabaya? Umeona umenyimwa haki/umeonewa,Basi leo Yesu anatwambia twende kwake

Sehemu ya mahubiri ya Askofu Eusebius Nzigirwa wakati wa Misa ya Sikukuu ya Kupaa Bwana tarehe 14-05-2015 St. Peters Oysterbay Alisisituza mambo makuu manne tunayopaswa kufanya ili Yesu akirudi atukute tukiwa salama.

Mambo mawili kati ya manne aliyataja kutoka Injili ya Marko 1:1: Wakati umewadia, ufalme wa mbinguni umekaribia, tubuni na kuiamini injili. Mambo hayo mawili ni kutubu na kuiamini injili.

1. Kutubu
Akisema tutubu  anamaanisha Mungu anajua sisi sote ni wakosefu kwahiyo akisema tutubu maana yake ni kwamba tukiri kwamba sisi ni wakosefu (tuungame mara kwa mara). Tusiweke akiba ya madhambi mioyoni mwetu (Baba Askofu alitoa mfano wa usemi maarufu wa kidunia unaosema tulikuja duniani bila kitu tutarudi bila kitu -lakini ukweli ni kwamba mara nyingi tusipotubu tukifa tunarudi na mizigo ya dhambi. Kumbe tutubu ili tukifa hapa duniani turudi kwake bila madhambi lakini wema tuliotenda utaambatana nasi.

SWALI: TAJA SABABU AMBAZO UNADHANI ZINACHANGIA KUWAFANYA VIJANA WASIUNGAME KWA PADRI?
  
2. Kuiamini Injili
Ni kusikia sauti ya Mungu na kutenda maagizo yake, kama ambavyo unasikia sauti inakukumbusha kwenda kanisani, kutenda mema n.k. Kuna sauti nyingi sana hasa kipindi hiki cha utandawazi ambazo sio sauti ya Mungu mfano kutamani yasiyofaa, kuiga mitindo isiyoendana na maadili yetu, kuangalia picha mbaya, kusoma mambo yanayochochea mapenzi na vitu kama hivyo.

Jambo la tatu linatoka katika Injili ya Mathayo isemayo Njooni kwangu ninyi mliobarikiwa na baba yangu kwa sababu nilipokuwa na njaa ulinilisha, nilipokuw ana kiu ulininywesha.
SWALI: KATIKA HALI YAKO YA UJANA NI SAUTI GANI ZINAKUSUMBUA ZAIDI NA KUKUZUIA KUSIKIA SAUTI YA MUNGU?

3. Kutenda matendo ya huruma -
Luka 16:1-12 mfano wa hakimu dhalimu
Luka 16: 19-31 mfano wa Tajiri na Maskini Lazaro
Tunaona kwamba matendo ya huruma yanauwezo wa kumuondolea mtu adhabu anayostahili au kumpeleka mbinguni kabisa.

SWALI:
ORODHESHA MATENDO YA HURUMA AMBAYO KIJANA ANAWEZA KUYAFANYA KATIKA ULIMWENGU HUU WA UTANDAWAZI.

4. Tuwe watu wa msamaha
Sala aliyotufundisha Bwana wetu Yesu Kristo inatufundisha juu ya hili. Baba yetu uliye mbinguni...........utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea (Mathayo 6: 9-13). Na Mwinjili Marko inasisitiza juu ya kusamehe tukitaka kusali kwa kuwa Mungu anajua makwazo yapo siku zote duniani…. anasema ”Nanyi kila msimamampo na kusali, sameheni mkiwa na neno juu ya mtu: ili na Baba wa mbinguni awasamehe ninyi makosa yenu” Marko 11:25.

SWALI. JE NIMAMBO GANI UMEWAHI KUKUTANA NAYO NA UKASHINDWA KUSAMEHE AU UNADHANI UMESAMEHE LAKINI UKIKUMBUKA UCHUNGU UNARUDI NDANI KWA UPYA?
                       






                       







Maoni 3 :

  1. Mungu awabariki sana ni Mimi Frt.John

    JibuFuta
  2. nimependezwa na chapisho hili MUNGU hawaarikini sana

    JibuFuta
  3. Nimefurahishwa na chapisho hili. Mungu akubariki sana. Naomba niruhusiwe kulitumia kufundisha vijana

    JibuFuta